You are currently viewing Sheikh Basaleh afariki dunia, kuzikwa kesho

Sheikh Basaleh afariki dunia, kuzikwa kesho

Dar es Salaam. Mwanazuoni na sheikh maarufu Maalim Basaleh amefariki dunia leo Jumapili katika Hospitali ya Aga Khan alipokuwa akipatiwa matibabu akisumbuliwa na matatizo ya figo na saratani.

Mtoto wa marehemu Abdullatif Ali Basaleh amesema baba yake amefariki saa 12 jioni baada ya kulazwa kwa takribani wiki mbili na nusu akipatiwa matibabu hayo.Amesema mazishi ya baba yake yatafanyika kesho saa 7 mchana katika makaburi ya Kisutu.

“Leo baba amefariki dunia si muda mrefu kesho tutakwenda kumpumzisha baada ya swala ya Adhuhuri,” amesema Abdullatif.

Rafiki wa karibu wa Basaleh, Sheikh Issa Ponda ameliambia Mwananchi kuwa mwanazuoni huyo alikuwa amebobea katika masuala ya dini na kijamii.Amesema Sheikh Basaleh amewahi kuwa mwalimu wa shule za sekondari Unguja.

“Aliwahi kuwa mhadhiri mkubwa wa Kiislamu, baada ya kufariki Sheikh Abood Maalim yeye ndiye alibaki akiongoza mihadhara linganishi yaani hoja tofauti za itikadi mbalimbali. Atakumbukwa zaidi namna alivyopigania watoto wa kike kuvaa hijabu shuleni na Rais wa wakati huo (Ali Hassan Mwinyi), akaridhia.

” Haikuwa kazi ya kufanikiwa katika hili kwasababu alipata misukosuko kwa sababu yalifanyika maandamano aliyoyaongoza.Alikamatwa na polisi na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, lakini mwisho wa siku vazi liliruhusiwa,” amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda ambaye ni Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu Tanzania, amesema watu watakusanyika katika msikiti wa Maamur Upanga kisha kwenda makaburi ya Kisutu.Amesema Sheih Basaleh amejijengea umaarufu mkubwa ndani ya nje ya nchi.

“Sheikh Basaleh alikuwa na uwezo wa kufanya kazi kubwa katika jamii ikiwemo kujenga uelewa kwa wananchi.Tumeondokewa na mtu muhimu bara na visiwani,” amesema Sheikh Ponda.

Kwa mujibu Sheikh Ponda, Basaleh amezaliwa mwaka 1947 mjini Unguja amesomea Zanzibar na kufanya kazi ya ualimu akifundisha masomo ya Kiingereza na Kiarabu.

Shirikisha