You are currently viewing WARAKA WA WAZI KWA RAIS WA ZANZIBAR MHESHIMIWA DK HUSSEIN ALI MWINYI

WARAKA WA WAZI KWA RAIS WA ZANZIBAR MHESHIMIWA DK HUSSEIN ALI MWINYI

Kwako ndugu Rais

Uhusiano wako na mfanyabiashara Jitesh Ladwa ni wa muda mrefu. Binadamu lazima awe na marafiki na hii haki yako Mheshimiwa Rais wala si jambo baya. Isicho haki ni matumizi ya nafasi yako kama kiongozi wa umma tangu ukiwa Waziri wa Ulinzi (SMT) kufanya ufisadi na kuuficha kupitia rafiki yako bwana Jitesh na wengine.Naomba kukukumbusha kuwa taarifa za wewe na Jitesh kuendesha kampuni ya Kifaru Holdings kuingiza jeshini magari ya Ashok Leyland i wazi kwenye faili lako la maadili. Miaka yote ukiwa Waziri wa Ulinzi umeuzia jeshi magari kwa bei karibu mara mbili ya bei ya soko na wewe na Jitesh mmekwiba mabilioni ya shilingi. Uadilifu ungefuatwa tungeokoa mabilioni na kuimarisha maslahi ya wanajeshi wetu wanaofanya kazi kubwa ya kizalendo.

Majuzi Waziri wako wa Utalii bwana Simai kajiuzulu. Tatizo unajua linaunganika na rafiki yako Jitesh. Zanzibar ina maadili yake na imejenga utaratibu wake kisheria kubalansi uingizaji wa pombe kwa watalii na udhibiti wake kwenye jamii. Utaratibu huu wa kisheria ambao umeukuta ulipokuja hapa Zanzibar ulifanywa kwa kushirkisha wadau wa dini na jamii na kukubaliwa na umedumu kwa ufanisi.Umekuja Zanzibar umetaka kubadili utaratibu kiholela kwa maslahi yako wala si jamii ya Wazanzibari. Hakuna asojua lengo lako ni kina Jitesh kuingiza pombe Zanzibar na mwingizaji mkuu ni wewe, wao ni washirika. Mheshimiwa Rais muda umefika uache kushinda miskitini kinafiki na kujipambanua wazi wewe ni mtu wa namna gani.

Kabla ya kumalizia nataka kukumbusha kwa nini hayati Rais Magufuli alifuta maduka yasiyo na ushuru kwenye kambi za jeshi. Unakumbuka? Alikusamehe kwa heshima ya baba yako kwani kwa miaka mingi ukiwa Waziri wa Ulinzi ulitumia maduka hayo na wenzako kina Jitesh kujinufaisha kwa kutolipa ushuru! Uhujumu uchumi. Magufuli akaamua asikutie aibu ayafutilie mbali. Hapa Zanzibar pia ulitumia maduka yale ukiwa Waziri wa Ulinzi kuingiza pombe kupitia kampuni ya Mohans. Zikawa hazilipiwi kodi stahiki, udhibiti hovyo, zikasambaa hata nje ya maeneo ya biashara kinyume na utaratibu wa jamii yetu. Biashara ya pombe kwako si mpya Mheshimiwa Rais! Tunakukumbusha tu kwamba haya yanafahamika maana kuna wakati binadamu unaweza kusahau.

Mwananchi wako
Fahad Kombo (Chambucho)
0777 632 801
Kisiwa Panza

Shirikisha