You are currently viewing Kada wa CCM Zanzibar apotea kwa miaka miwili. Familia yataka majibu

Kada wa CCM Zanzibar apotea kwa miaka miwili. Familia yataka majibu

Zanzibar. Familia ya kada mkongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Juma Juma Makame ambaye amepotea kwa zaidi ya miaka miwili inahitaji majibu kutoka kwa vyombo vya ulinzi vya Zanzibar, wakieleza kuwa suala hilo limechukua muda mrefu huku ukimya unaoendelea ukiwatia wasiwasi mkubwa.
Makame alitoweka Agosti 19, 2020, takribani miezi miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu, alipo kwenda kwenye mazoezi, kama kawaida yake akikimbia na kuogelea katika eneo la Mazizini mjini Unguja. Hakuonekana tena akiacha familia na marafiki katika simanzi kubwa.

Makame ambaye amefikisha umri wa miaka 66 mnamo Februari 2, 2023, alipotea katika hali ya kutatanisha punde baada ya kuwa mshindi wa pili katika kinyang’anyiro cha kura za maoni za CCM za kugombea uwakilishi wa jimbo la Chaani.
Kupotea kwa Makame kunakuja wakati kukiwa na tetesi za rushwa katika uchaguzi wa ndani uliohusisha wagombea tisa ambapo kulimfanya Makame kuonesha nia ya kukata rufaa juu ya matokeo yaliyompa ushindi Nadir Abdullatif Yussuf Alwardy  ambaye kwa sasa ni mwakilishi wa Chaani.

Familia ya Makame iliieleza Zanzibar Leaks kuwa wameamua kuongea kuhusu hatma ya mpendwa wao huyo baada ya kuona wamekuwa wakipokea ushirikiano usioridhisha kutoka kwa mamlaka husika juu ya alipo mpendwa wao.
“Hakuna linaloshindikana Serikali ikiamua,” anaeleza Fatma Juma Makame, dada wa Makame katika mahojiano na Zanzibar Leaks. “Tunaamini sababu zinazofanya tusijue chochote kuhusu kaka yetu ni kwa sababu Serikali hawajalipa uzito suala hili.”
Suala linalomchanganya zaidi Fatma ni kuwa kaka yao amekuwa mtumishi serikalini kwa miongo mingi, jambo analoelezea kuwa “siyo haki kabisa.”

“Kaka yangu alikua ni mtumishi wa umma mchapa kazi katika maisha yake yote,” anaelezea Fatma. “Inakuaje Serikali aliyoitumikia hailipi kipaumbele hili suala la yeye kupotea? Sidhani kama ni haki kabisa.”
Tulimuuliza Kamishna Msaidizi wa Polisi Zanzibar Richard Tadei Mchomvu ikiwa kama polisi wanalifahamu suala hili, ambapo alieleza kuwa polisi wanaifahamu kesi hiyo na kuwa bado wanaendelea na uchunguzi.
“Bado tunamtafta sehemu mbalimbali,” anaeleza Mchomvu katika mahojiano. “Hata hivyo, jitihada zetu bado hazijazaa matunda. Lakini bado tunaendelea na upelelezi na tutuwajulisha umma tutakapopata taarifa zozote mpya.”

Picha ya Juma Makame iliyopo nyumbani kwake

Mtumishi wa umma wa muda mrefu
Makame ambaye ni mume kwa wake wawili Samira Salum na Mwajuma Mkuya alistaafu utumishi wa umma mwaka 2019 akifanya kazi kama Kamishna Msaidizi wa Kampuni ya Bima ya Zanzibar (ZIC), hii ikiwa ni miaka 43 katika utumishi wa Serikali.
Alipata Shahada ya Uzamili katika fedha mwaka 1993 katika chuo cha Strathclyde, kilichopo katika jiji la Glasgow nchini Scotland. Aliingia rasmi katika utumishi mwaka 1976, akianza kama mwalimu kabla ya kushika nafasi mbalimbali serikalini.

Wakati akiwa serikalini Makame alishika nyadhifa mbalimbali katika chama kama mjumbe wa kamati za mkoa na wilaya na katika Jumuiya ya Wazazi jimbo la Chaani.
Samira Salum, ambaye ni mke mdogo wa Makame, anamuelezea mume wake huyo kama mtu mkarimu aliyeipenda familia yake sana.
“Hakuwa mume pekee, alikua mlinzi na mlezi wetu,” anaelezea Samira, mama wa miaka sitini mwenye watoto saba. “Sasa hatujui mume wangu yuko wapi, kama ni mzima au amekufa.”

Simai Abdallah Juma ni rafiki wa Makame kwa zaidi ya miaka thelathini na pia ni dereva wake binafsi, anayemuelezea Makame kama “mtu wa watu” ambapo kupotea kwake kumemuachia simanzi nzito.
“Alikua ni zaidi ya bosi kwangu, alikua ni rafiki wa shida na raha, ndugu anayejali, ” Juma aliiambia Zanzibar Leaks katika mahojiano. “Miaka hii miwili bila ya uwepo wake imekuwa ni migumu zaidi maishani mwangu. Namkumbuka sana natamani angekuwa na sisi hivi sasa.”

‘Tuliona gari lake tu’
Siku ya Agosti 19, 2020, ingekuwa kama siku zingine katika maisha ya Samira Salum lakini habari mbaya alizopokea kuhusu mume wake zilibadilisha kabisa siku hiyo.
Ilivyofika jioni, Samira alianza kupata wasiwasi hasa baada ya mume wake kuchelewa sana kurudi nyumbani.
Kwa kawaida Makame husali sala ya maghrib nyumbani kwake, na muda ulienda kufikia saa moja na nusu usiku na Makame alikua bado hajarudi.

Mke wa Juma Makame, Samira akiangalia picha waliyopiga pamoja

 

“Kwa kuhisi kama kuna kitu kibaya, niliwaambia watoto kuwa baba yao hajarudi nyumbani,” anaeleza Samira. “Tulienda Mazizini ambapo hufanya mazoezi yake lakini tuliishia tu kulikuta gari lake limepakiwa na ufunguo ukiwa umeachwa lakini yeye hakuwepo.”
Waliwauliza watu mbalimbali ambao waliwaeleza kwamba wakati walimuona Makame akitoka majini hawakumbuki alielekea wapi. Jitihada za familia za kutaka mamlaka kuonyesha video za CCTV hazikufanikiwa.

Mwajuma Mkuya Suleima, mke mkubwa wa Makame, anaieleza Zanzibar Leaks kuwa alivyosikia tu habari za kupotea kwake alikumbuka kitu mume wake huyo alimwambia na ambacho anadhani ndio sababu za kupotea kwake.
“Kabla ya kupotea, mume wangu alipokea meseji iliyomjulisha kuwa uchaguzi wa ndani wa chama ulishamiri rushwa na kwamba inabidi apiganie haki yake,” anaelezea Mwajuma, mama wa watoto watano.
Siasa za chama
Kupitia mahojiano tuliyofanya na baadhi ya wagombea walioshiriki uchaguzi wa ndani wa CCM na Makame, Zanzibar Leaks imegundua kuwa mwanasiasa huyo alipotea wakati akipanga kukata rufaa juu ya maamuzi ya chama kumtangaza Nadir kama mshindi wa kura za maoni kugombea uwakilishi wa jimbo la Chaani.
Khamis Juma Ali alikuwa ni mgombea aliyekuwa wa tatu nyuma ya Makame. Ali, 55, aliiambia Zanzibar Leaks kuwa Makame aliwasiliana naye na kumuambia hakufurahishwa na matokeo na kwamba alipanga kukata rufaa kwa ngazi za juu za maamuzi ndani ya CCM.
“Baada ya tetesi kusambaa kuwa Makame atachukua nafasi ya Nadir kama mgombea wa CCM Chaani, Nadir aliitwa Dodoma kabla Kamati Kuu ya chama haijafanya maamuzi ya mwisho,” Ali aliiambia Zanzibar Leaks katika mazungumzo.
“Ni katika kipindi hicho ndipo Makame alipotea na tetesi zikaanza kusambaa kuwa nitaweza kutangazwa kuwa mgombea [kama chama kikifuta ushindi wa Nadir],” alifafanua. “Nilipoteza usingizi kwa siku kadhaa, sikutaka kuwaacha watoto wangu bila baba, na namshukuru Mungu hilo halikutokea.”

Maelezo ya Ali yanaendana na maelezo ya Othman Khamis, Kapteni mstaafu wa MV Mapinduzi na rafiki wa karibu wa Makame aliyeiambia Zanzibar Leaks kuwa ni kweli rafiki yake alipanga kukata rufaa.
“Alinipigia na kuniambia kuna ishara kuwa rufaa yake itashinda na bado ana matumaini ya kuongoza Chaani,” Khamis, 55, alieleza katika mahojiano. “Kabla hilo halijatokea, alipotea. Hatujamuona kwa muda mrefu sana, ninapoteza matumaini kama tutamuona tena.”
Lakini Mula Othman Mula ambaye alikua ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kaskazini Unguja na msimamizi wa uchaguzi katika uchaguzi wa ndani anapinga hoja hizo, akieleza kuwa Makame hajawahi kulalamika kuhusu matokeo ya uchaguzi na hakuwa na mpango wa kukata rufaa.
“Hauwezi kukata rufaa bila kunijulisha,” anaeleza Bwana Mula. “Makame hakuwahi kuandika kwangu kulalamikia uchaguzi. Hakuwahi hata kupiga simu kuuliza chochote kuhusu uchaguzi. Hakujawahi kuwa na kitu kama hicho.”
Mula anaeleza wakati anafikiri siasa zinaweza kuwa sababu ya kupotea kwa Makame, mara ya mwisho alivyofuatilia aligundua pia alikua na migogoro na watu mbalimbali ambao aliwapa fedha kwa ajili ya kufanya biashara.
Katika mazungumzo na Zanzibar Leaks, Nadir Abdullatif Yussuf Alwardy, ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, amezipinga taarifa za uwepo wa rushwa katika uchaguzi wa ndani wa kupata mgombea wa CCM jimbo la Chaani.
Pia, amekataa kuwa aliitwa na CCM Dodoma siku chache kabla ya kupotea kwa Makame, akieleza kuwa hajawahi kuitwa na chama chake na hakuwahi kusafiri kwenda Dodoma katika hicho kipindi.
Lakini anakubali watu wengi wanamnyooshea kidole juu ya kupotea kwa Makame, huku wakimshutumu kuwa anahusika na upoteji wake, jambo ambalo analikataa vikali.
“Nimehojiwa na polisi kuhusu kuhusika katika hilo tukio, mara zote nimeeleza sifahamu lolote kuhusu hilo,” Nadir anaiambia Zanzibar Leaks. “Sikuwahi kugombana naye, hakuna namna yeyote ninaweza kuhusika na kupotea kwake.”
Nadir anatoa wito kwa vyombo vya uchunguzi Zanzibar kuharakisha uchunguzi ili umma uweze ufahamu nini hasa kilitokea, akisisitiza kwamba yeyote anayehusika katika tukio hilo—“hata kama ni mimi” —lazima akutane na mkono wa sheria.

Katika mfululizo wa matukio yaliyotokea juu ya sakata hili, mnamo Septemba 9, 2020, aliyekuwa Naibu Katibu wa CCM (Zanzibar) Dk Abdallah Juma Mabodi alimtaja Makame, akisema:
“Tunamuombea ndugu yetu Juma wa Juma [Makame] Mwenyezi Mungu ampe subira huko alipo. Inshallah tutakuwa naye kipindi kifupi kijacho. Tumuombeeni dua sote.”
Dk Mabodi alikuwa akiongea katika hafla ya kuwapongeza wagombea ambao wameidhinishwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa nchi kupitia tiketi ya CCM.
Watu wengi ikiwemo familia ya Makame na wagombea wenzake, wanaamini kauli ya Mabodi ni ushahidi kuwa chama kitakuwa kinajua nini kilimkuta Makame.

Makame akipokea fomu za ugombea wa uchaguzi wa kura za maoni CCM

 

Zanzibar Leaks ilimuuliza Dk Mabodi, ambaye alikuwa bado wakati huo ni Naibu Katibu Mkuu CCM (Zanzibar), kuwa alimaanisha nini aliposema watakuwa na Makame kipindi kifupi kijacho ambapo hakuweza kutoa majibu ya moja kwa moja.
Badala yake, Dk Mabodi alieleza kuwa hakuna ambaye angependa mpendwa wake kupotea kwa miaka na kuombea kwamba Makame apatikane na kuungana na familia yake.
“Kama siyo kauli ya Dk Mabodi, tungeridhika kuwa labda baba yetu alizama majini na kufariki,” anaeleza Leyla Juma, mtoto wa Makame akiongea na Zanzibar Leaks. “Ni kauli iliyotuacha na maswali mengi.”

Matumaini yasiyofifia
Samira Salum, mke mdogo wa Makame, haamini kuwa mme wake amefariki, huku akitumaini kwamba atarudi siku moja.
“Hajafa,” anaeleza Samia katika mahojiano. “Moyo wangu unakataa kuwa mume wangu kafariki. Naamini yuko sehemu mzima. Natumaini atarudi.”
Samira na mke mwenzake Mwajuma wamekataa ushauri wa Ofisi ya Mufti Zanzibar kuwa wakae eda, wakisema ni kitu hawatakubali.
Eda ni kipindi ambacho wanawake wa Kiislamu hukaa baada ya kufariki kwa mume  au baada ya talaka, ambapo katika kipindi hicho hataruhusiwa kuolewa na mwanaume mwingine.
“Sitakaa eda mpaka nijue nini kimemkuta mume wangu,” Mwajuma Makame anaeleza. “Najua mume wangu hajafa. Najua atarudi tuje kusaidiana kulea watoto.”

Shirikisha